JKCI Kutambulika Kimataifa kwa Kazi Bora za Upasuaji wa Moyo
Huduma bora za matibabu pamoja na upasuaji wa
moyo zimeifanya Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) kutambulika kimataifa na
hivyo wataalamu wengi kutoka nje ya nchi kuvutiwa kwenda kufanya kambi maalum za matibabu ya moyo kwa kushirikiana na madaktari wa
Taasisi hiyo.
Hayo
yamesemwa leo na Mwakilishi wa Mufti,Sheik
Hassan Said Chizenga wakati wa hafla fupi ya kuwashukuru
wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Kimataifa ya
Kiislamu ya Misaada (IIRO) ya nchini
Saudi Arabia ambao wako JKCI katika kambi maalum ya upasuaji wa moyo.
Sheik Chizenga alisema Taasisi ya Moyo imekua kimbilio kwa wagonjwa wa Afrika na Dunia nzima kwa ujumla kutokana na
huduma bora za matibabu ya moyo zinazolewa kiufanisi.
“Taasisi hii imekua kioo si kwa Afrika tu
bali Dunia nzima kwa kutoa huduma ya matibabu ya Afya ya moyo na upasuaji kwa
wagonjwa ambao ni watanzania na wengine kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati”
,alisema Sheik Chizenga.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete Agnes Kuhenga aliishukuru nchi ya Saudi Arabia kwa ushirikiano inaouonyesha
kwa Serikali ya Tanzania katika kuimarisha utaalam na kuboresha utoaji wa
huduma za afya hapa nchini.
“Ushirikiano wa Tanzania na Saudi Arabia
umelenga kuhakikisha watanzania wanakuwa na afya bora na kuweza kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kulifanya taifa letu kufikia
lengo la kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025”, alisema Kuhenga.
Naye Naibu Balozi wa Saudi Arabia nchini,
Mhe. Ahmed Al Ghamidi alisema katika kambi hiyo wataalamu kutoka nchi zote
mbili wameweza kuunganisha nguvu na ujuzi waliokuwa nao na kufanya matibabu kwa
wagonjwa.
Mhe.Balozi Ghamidi alisema, “Katika kambi hii
ya siku saba maisha ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji yameweza kuokolewa na pindi watakapopona watarudi nyumbani na kuendelea
na majukumu yao ya kazi za kila siku”,.
Katika kambi hiyo jumla ya wagonjwa 20
wanatarajia kufanyiwa upasuaji wa moyo wa
kufungua kifua na kubadilishwa valvu
zaidi ya mbili ambapo hadi leo wagonjwa
14 walishafanyiwa upasuaji na hali zao zinaendelea vizuri.
Comments
Post a Comment