JKCI yawafanyia upasuaji wa Moyo wagonjwa 36 bila kufungua kifua

Jumla ya wagonjwa 36  wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua na bila kufungua kifua katika kambi maalum ya matibabu inayofanyika katika Taasisi ya Moyo  Jakaya Kikwete (JKCI).
Upasuaji huo unafanywa na madaktari bingwa wa moyo wa Taasisi hiyo kwa kushirikiana na wenzao wa Shirika la Albalsam  Care & Care la nchini Saudi Arabia ambapo wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa kufungua kifua ni 10 na bila kufungua kifua kwa kutumia mtambo wa Cathlab kwa njia ya kutoboa tundu dogo katika  paja 26.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu Bashir Nyangasa alisema wagonjwa waliofanyiwa upasuaji hali zao zinaendelea vizuri na wengine wameshatoka katika chumba cha uangalizi maalum na kurudi wodini kwa ajili ya kufanya mazoezi pamoja na matibabu.
 “Tunafanya upasuaji wa kubadilisha valvu kwa wagonjwa ambao  valvu zao hazifanyi kazi vizuri, kubadilisha mishipa ya moyo inayosafirisha damu kutoka mishipa mikubwa kwenda kwenye mzunguko wa moyo na kuziba matundu kwenye moyo kwa watu waliozaliwa na matundu hayo”,.
“Katika kambi hii tumemfanyia upasuaji wa kupandikiza mshipa wa damu kutoka kwenye mguu na kuuweka kwenye moyo mgonjwa aliyekuwa na maradhi mawili ya moyo ambayo  ni kuziba kwa mishipa ya damu na mlango mkubwa wa moyo”, alisema Dkt. Nyangasa.
Dkt. Nyangasa aliwashauri wananchi wasingojee kuumwa ndio waanze kutafuta bima za afya bali wajenge mazoea ya kuwa na bima za afya kwani mwili ni kama gari linalopelekwa gereji mara kwa mara kwa ajili ya ukarabati vivyo hivyo mwili unatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kuepuka vifo vya ghafla.
Kwa upande wake  daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kutoka Shirika la Albalsam Care and Care la nchini Saudi Arabia Emad Bukhari aliipongeza  Serikali ya Tanzania kwa kuwekeza  katika vifaa vya kisasa vya matibabu ya moyo.
Dkt. Emad Bukhari alisema ,“Kuwepo kwa mashine hizi za kisasa, wataalam pamoja na huduma nzuri  za kibingwa katika Taasisi hii, kumeifanya  kutambulika kimataifa na  hivyo kuzifanya taasisi zinazotibu magonjwa ya moyo Duniani kuja mahali hapa kutoa huduma kwa wananchi”, .
Kambi hiyo ilienda sambamba na utoaji wa elimu pamoja na ubadilishanaji wa ujuzi wa kazi ambao umewajengea uwezo madaktari, wauguzi pamoja na wataalamu wa mashine za moyo

Comments

Popular posts from this blog

Balozi wa Uholanzi nchini Mhe. Jeroen Verheul aipongeza Taasisi ya Moyo Nchini

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Shirika la Balsam Care & Care la nchini Saudi Arabia wakimfanyia mgonjwa upasuaji wa kuzibua mishipa ya moyo bila kufungua kifua

Katika kuadhimisha siku ya moyo Duniani tarehe 29/09/2018 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari wa Moyo Tanzania (THF) wafanya upimaji na utoaji wa elimu ya afya ya moyo bila malipo katika viwanja vya Hospitali ya Vijibweni iliyopo wilaya ya Kigamboni.

JKCI Kutambulika Kimataifa kwa Kazi Bora za Upasuaji wa Moyo