Balozi wa Uholanzi nchini Mhe. Jeroen Verheul aipongeza Taasisi ya Moyo NchiniTaasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepongezwa kwa jitihada zake inazozifanya  za  kuweza kuwafikia wananchi wengi  kwa  kutoa huduma bora za matibabu, elimu na ushauri wa jinsi ya kuepukana na magonjwa ya  moyo.
Pongezi hizo zimetolewa jana na Balozi wa Uholanzi nchini Mhe.  Jeroen Verheul  alipokuwa  akiongea na wafanyakazi wa Taasisi hiyo wakati wa ziara yake ya kuangalia huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa kwa wagonjwa.
 Mhe. Verheul alisema Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ni moja ya Taasisi zinazofanya kazi vizuri ya kutoa huduma ya matibabu ya moyo  katika nchi zilizopo Kusini mwa Afrika .
Kuhusu Ubalozi wake  kushirikiana na Taasisi hiyo katika utoaji wa huduma kwa wananchi alisema ataangalia ni jinsi gani watashirikiana  katika programu  mbalimbali za afya ambazo zinatolewa  hapa nchini kupitia  Ubalozi wa Uholanzi.
“Wiki tatu zijazo nitaenda nchini Uholanzi ambako tuna mkutano wa mabalozi wote. Kupitia mkutano huo nitaangalia ni Taasisi ipi ambayo itaweza kuja nchini kufanya matibabu ya moyo kama ilivyokuwa kwa nchi zingine ambazo zinatuma wataalamu wake kuja  katika Taasisi hii kutoa huduma za matibabu kwa wananchi”,alisisitiza Mhe. Verheul.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi alimshukuru Mhe. Balozi kwa kuwatembelea na kuona huduma mbalimbali wanazozitoa  na kusema kuwa wanajitahidi kuhakikisha kila mwananchi anayefika katika Taasisi hiyo anapata huduma bora za matibabu ya moyo.
Alisema idadi ya wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo imekuwa ikiongezeka kila mwaka ukilinganisha na miaka ya nyuma hii inaonyesha kuwa hivi sasa wananchi wenye matatizo ya moyo wanaelewa ni wapi pa kwenda kutibiwa magonjwa hayo.
“Kutokana na wataalamu wetu kuwa na utaalamu wa kutosha na hospitali kuwa na vifaa vya kisasa tumeweza kufanya upasuaji kwa wagonjwa wengi zaidi kwa mwaka 2018 ukilinganisha na mwaka 2017”.
“Mwaka 2018 tumefanya upasuaji wa kufungua kifua kwa wagonjwa 1053 na bila kufungua kifua kwa wagonjwa 405 ambapo mwaka 2017 tulifanya upasuaji wa kufungua kifua kwa wagonjwa 225 na bila kufungua kifua kwa wagonjwa 800”, alisema Prof. Janabi.

Akiwa katika Taasisi hiyo Mhe. Balozi Verheul alitembelea maabara ya uchunguzi wa matatizo na tiba za magonjwa ya moyo (Cath Lab), jengo jipya la watoto ambalo ukarabati wake ukikamilika   litakuwa na vitanda  32 na vitanda tisa katika  chumba cha wagonjwa walioko katika uangalizi maalum (ICU), wodi ya watoto na wagonjwa waliofanyiwa na wanaosubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua,  chumba cha upasuaji na chumba cha wagonjwa walioko katika uangalizi maalum (ICU).
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi na  Balozi wa Uholanzi nchini Mhe.  Jeroen Verheul  pamoja na wafanyakazi wa Taasisi hiyo wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya  kumaliza kwa ziara ya Mhe. Balozi  ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa  kwa wananchi.

Comments

Popular posts from this blog

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Shirika la Balsam Care & Care la nchini Saudi Arabia wakimfanyia mgonjwa upasuaji wa kuzibua mishipa ya moyo bila kufungua kifua

Katika kuadhimisha siku ya moyo Duniani tarehe 29/09/2018 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari wa Moyo Tanzania (THF) wafanya upimaji na utoaji wa elimu ya afya ya moyo bila malipo katika viwanja vya Hospitali ya Vijibweni iliyopo wilaya ya Kigamboni.

JKCI Kutambulika Kimataifa kwa Kazi Bora za Upasuaji wa Moyo

JKCI yawafanyia upasuaji wa Moyo wagonjwa 36 bila kufungua kifua